MBUNGE wa Viti Maalumu, Vicky Kamatta (CCM), amekanusha habari zilizoripotiwa leo na gazeti moja la hapa nchini kuwa amek...
MBUNGE wa Viti Maalumu, Vicky Kamatta (CCM), amekanusha habari
zilizoripotiwa leo na gazeti moja la hapa nchini kuwa amekamtwa na
Polisi Mkoa wa Dodoma kwa tuhuma za kuwatumia ujumbe mfupi wa simu za
matusi wabunge wenzake.
Habari zilisema kwa kipindi cha miezi kadhaa Vicky amekuwa akituma sms
za matusi kwa wabunge wenzake wa viti maalumu kupitia CCM, Catherine
Magige na Lucy Mayenga ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Uyui.
Taarifa zaidi zinasema kuwa wabunge hao walikuwa wakitumiwa sms za
matusi kwa namba ambapo baada ya kuona hali imekuwa ikizidi waliamua
kwenda kufungua jalada la malalamiko katika Kituo Kikuu cha Kati mjini
Dodoma na kuomba ufanyike uchunguzi ili waweze kumbaini mwenye namba
hizo. Kutokana na maelezo hayo, Jeshi la Polisi lilianza kufanya
uchunguzi kuhusu sakata hilo na kubaini namba hiyo imesajiliwa kwa jina
la mdogo wa kiume wa Vicky.
Baada ya Jeshi la Polisi kufuatilia, ilibainika namba hiyo ilikuwa ya mbunge huyo ingawa hakuisajili kwa jina lake.
Hata hivyo akijibu tuhuma hizo alisema kuwa anashangazwa na habari hizo
kwani hajakamatwa na polisi na kwamba alikuwa akijiandaa kwenda bungeni.