Tanzania ina wanachama hai zaidi ya 600 wa kundi la watu wenye imani ya siri ya Freemas...
Tanzania
ina wanachama hai zaidi ya 600 wa kundi la watu wenye imani ya
siri ya Freemasons wakiwa wanatokana na watu wa kada
mbalimbali wakiwemo maarufu, huku ikielezwa kwamba miongoni
mwao hakuna viongozi wakuu wa serikali.
Hayo
yalibainishwa na Kiongozi wa kundi la Freemasons katika eneo
la Afrika Mashariki, Jayantilal Keshavji Chande maarufu kama
Sir Andy Chande.
Kiongozi
huyo Mtanzania mkazi wa Dar es Salaam mwenye asili ya Kiasia,
alisema licha ya Tanzania kuwa na wanachama hao, kwa sasa idadi
ya wanachama duniani inapungua tofauti na inavyoonekana sasa
kuwa wanaongezeka kutokana na kuibuka maneno mengi kuhusu kundi
hilo.
Alisisitiza kuwa si
rahisi kumjua mwanachama wa kundi hilo, bali wenyewe ndio
wanaofahamiana, akisema ni siri na kwamba wenyewe wanakutana
katika vikao mbalimbali mara moja kwa mwezi au zaidi.
Alisema
nchini kuna wanachama zaidi ya 600 wakiwemo wafanyabiashara,
watumishi serikalini, walimu pamoja na wanataaluma mbalimbali
wanaoheshimika sana na kusisitiza kuwa kuna maneno mengi
yanayosemwa kuhusu kundi hilo, ambayo siyo ya kweli.
Alisema
idadi ya wanachama wake duniani inazidi kupungua kutoka
milioni nane hadi sasa wako milioni sita, tofauti na wengi
wanaodhani kuwa idadi hiyo inaongezeka.
Chande
alizungumza na mwandishi wa habari hizi katika Shule ya
Sekondari ya Shaaban Robert ambako yeye ni Mwenyekiti wa Bodi
ya shule alipozungumzia maadhimisho ya miaka 50 tangu
kuanzishwa kwake.
Alisema
duniani kuna watu wazito wengi ambao ni wanachama wa kundi hilo
kama majaji wakubwa na hata Binamu wa Malkia Elizabeth wa
Uingereza ni kiongozi mkubwa wa kundi hilo.
Akizungumzia
masharti ya kujiunga na kundi hilo, Chande alisema ni lazima
mwanachama huyo awe anaamini katika Mungu bila kubagua iwapo ni
Mkristo au Muislamu.
Alisema
pia ni lazima anayetaka kujiunga awe na umri unaozidi miaka 21
na walio chini ya umri huo hawaruhusiwi kujiunga na lazima
familia ya anayetaka kujiunga na wanandugu wafahamu kuwa
umejiunga na kundi hilo.
"Unajua
katika imani hii kuna michango mbalimbali ambayo unatakiwa
kutoa ambayo ni zaidi ya dola milioni sita (karibu Sh bilioni
10), hivyo ni lazima ndugu wafahamu ili kuepuka matatizo
utakapotakiwa kutoa," alisisitiza.

Alisema
si kweli kuwa wenye fedha wengi ni wanachama wa kundi hilo
huku akikanusha wanachama wanajiunga kwa ajili ya kupata fedha,
bali ni dini kama imani nyingine.
Alisisitiza
kuwa hakuna ukweli kwamba wanaopata mafanikio katika maisha
wakiwa ndani ya imani ya Freemasons kuwa wanatoa kafara watu
wao wa karibu kwa lengo la kupata utajiri.
Chande
pia alisema hairuhusiwi kutumia jina la kundi hilo kwa nia ya
kujipatia nafasi sehemu mbalimbali au kuongeza nafasi katika
chuo au shule.