Malipo ya Sh15,000 anayodaiwa shule, yanaweza kuonekana kuwa ndio chanzo cha kupoteza mwelekeo kwa binti wa miaka 14, Rachel Sun...
Malipo
ya Sh15,000 anayodaiwa shule, yanaweza kuonekana kuwa ndio chanzo cha
kupoteza mwelekeo kwa binti wa miaka 14, Rachel Sunguya.
Lakini
hilo laweza kuwa ni jibu la haraka haraka; binti huyo amekimbia mila
potofu za unyanyasaji na ukatili dhidi ya watoto wa kike.
Kwa
sasa, Rachel, ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya
Sekondari ya Benjamin Mkapa iliyo wilayani Simanjiro, amekimbia nyumbani
kwao kukwepa ndoa ya lazima. Amehifadhiwa Arusha na msamaria mwema,
lakini hana uhakika wa kuendelea na masomo licha ya kuwa na nia ya dhati
ya kusoma.
“Kwa
zaidi ya wiki tatu nilikuwa nyumbani. Nilirudishwa kutokana na kudaiwa
mchango huo na nilipomwambia baba alipe, aligoma na baadaye nilimsikia
akipanga niolewe,” anasema wakati akisimulia mkasa wake.
Rachael anasema baba yake alimwambia kuwa ni lazima aolewe kwani hana fedha za kumlipia ada mtoto wa kike.
“Baada
ya kupata taarifa hii na kubaini kuna mipango ilikuwa inafanywa
niolewe, niliamua kukimbilia hapa Arusha Mjini ili kupata msaada wa
kuendelee na masomo,” anasema.
Anasema
katika familia yao, wapo watoto 15 na baba yake ambaye ni mfugaji,
mwenyeji wa Kata ya Komolo, Wilaya ya Simanjiro ana wake wanne.
“Mama yangu aliondoka nyumbani miaka mitano iliyopita na sijui alipo,” anasema.
Anasema
kwa mama yake, yeye alizaliwa peke yake na hana mdogo wake, ila kuna
watoto wengine wa kiume katika familia hiyo, wanaendelea na masomo.
“Yupo Baraka ambaye anasoma kidato cha tatu na amekuwa akilipiwa ada,” anasema.
Anasema
kwa sasa ataendelea kukaa Arusha, hadi hapo atakapopata msamaria mwema
ili kumsomesha kwa kuwa hataki tena kurejea nyumbani.
Apeleka malalamiko polisi
Jitihada
za mtoto huyo, kuomba kusaidiwa na Dawati la Jinsia katika Kituo Kikuu
cha Polisi, Arusha zilikwama, baada ya kutoa maelezo na kutakiwa kurejea
nyumbani wakati suala lake likifuatiliwa.
“Nimeenda
polisi, nimetoa maelezo, lakini, nimeambiwa nirudi nyumbani,
watafuatilia. Sasa, nitarudi vipi wakati hawataki nisome wanataka
niolewe mimi nimeamua kubaki mjini,” anasema.
Mtoto
huyo alisema kwamba anakumbuka akiwa darasa la tatu alichukuliwa na
wenzake na kwenda kufanyiwa tohara kwa nguvu, lakini licha ya kwenda
kulalamika polisi hakuna hatua zilizochukuliwa.
“Nakumbuka
kipindi kile tulilalamika polisi na wakaja nyumbani, lakini hakuna
hatua zilizochukuliwa badala yake mimi nilionekana adui katika familia
na hata kutengwa,” anasema.
Mwalimu mkuu azungumza
Mwalimu mkuu wa Shule ya Sekondari ya Benjamin Mkapa, Emanuel Karo anakiri kumfahamu mwanafunzi huyo anayesoma kidato cha pili.
Hata hivyo, anasema kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa hajaonekana shuleni na hajulikani alipo.
Anasema mwanafunzi huyo anatakiwa kujiandaa na mtihani wa kidato cha pili mwaka huu, ambao utafanyika mwezi ujao.
“Nashukuru
kwa kunipa taarifa hii kuwa huyu mtoto yupo huko Arusha. Sisi huku
hatujui wala wazazi wake hawajui alipo na hawajafika hapa kutoa taarifa
yoyote,” anasema.
Mwalimu
huyo, anatoa wito kusaidia mtoto huyo, wa kike ili aweze kufanya
mtihani wa kidato cha pili wakati taratibu nyingine zikifuatwa.
“Tunaomba
aletwe kufanya mtihani wa kidato cha pili kwani hatuna taarifa zake na
ni kweli amekuwa na matatizo ada na michango mbalimbali kutowasilishwa,”
anasema.
Mwalimu
anakiri kuwa wazazi wa mtoto huyo wamekuwa hawatoi ushirikiano kwa
uongozi wa shule kwa kulipa ada na michango, jambo ambalo linaathiri
maendeleo yake.
Mlezi aliyemhifadhi azungumza
Haruna
Idd, msamaria mwema, ambaye alimwokota mtoto huyo akiwa eneo la Kituo
cha Mabasi Arusha anasema: “Nilikuwa katika kazi zangu nikamuona huyu
binti amezungukwa na vijana. Baada ya kumhoji ndipo alinipa historia
yake,” anasema.
Anasema
mtoto huyo, alieleza kuwa ametoroka nyumbani, kwa kuwa anataka kuolewa
kwa nguvu na anataka msaada wa kusoma na hana ndugu yoyote hapa Arusha
Mjini.
“Baada ya maelezo hayo niliamua kumchukua ili kumuepusha na vijana ambao walikuwa tayari wameanza kumzengea,” anasema.
Hata hivyo, anasema yeye hana uwezo wa kumsomesha kwa kuwa hana fedha na kwa zaidi ya mwezi mmoja, amekuwa naye nyumbani kwake.
“Tunaomba
watu wenye uwezo wajitokeze kumsaidia kwa kuwa baada ya kumpeleka
polisi na alipotakiwa kurejea nyumbani kwao, aligoma,” anasema.