Msanii wa muziki wa kizazi kipya, Ali Salehe Kiba maarufu Alikiba, amezungumzia yaliyomsibu hata kujiweka kando ya shughuli za muziki na...
Msanii wa muziki wa kizazi kipya, Ali Salehe Kiba maarufu
Alikiba, amezungumzia yaliyomsibu hata kujiweka kando ya shughuli za
muziki na ujio wake mpya.
Kiba alijiweka kando ya muziki kwa muda wa miaka
mitatu, huku upande wa pili akikumbwa na skendo mbalimbali kuhusu maisha
yake binafsi.
Baadhi ya mambo hayo ni madai ya kuwa na uhusiano
wa kimapenzi na mwigizaji Elizabeth Michael(Lulu). Pia kuwapo kwa
taarifa za kusaini mkataba mkubwa na Kampuni ya Sony Music Africa
iliyopo nchini Afrika Kusini.
Lakini kubwa ni madai kwamba kupotea kwa Kiba
kumetokana na ujio na kukomaa kimuziki kwa msanii Naseeb Abdul (Diamond)
na vilevile wakidaiwa pia kuwa na ugomvi uliokosa suluhu.
Gazeti hili lilimtafuta Kiba kutaka kujua mambo
mbalimbali ikiwamo uhusiano wake na Diamond, ambapo katika gari yake
msanii huyo alikutwa akisikiliza nyimbo za msanii Diamond Plutnumz,
‘Mawazo’.
Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano hayo yaliyofanyika nyumbani kwa msanii huyo Kunduchi Beach.
Mwandishi: Naona unasikiliza nyimbo za Diamond kwa hisia, vipi uhusiano wenu, inadaiwa mna ugomvi mkubwa, tatizo nini?
Ali Kiba: Bifu langu na Diamond
limejengwa na vyombo vya habari na mitandao ya kijamii. Sijawahi
kumchukia, wala sidhani kama na yeye ilitokea kwake. Naona kuna wafuasi
wangu na mashabiki wanaozungumza hivyo kama maoni yao kwenye picha au
matukio yanayowekwa katika vyombo vya habari.
Mwandishi: Unamwelezeaje Diamond?
Ali Kiba: Ni mwanamuziki aliyeifanya Tanzania
ijivune kwa muziki mzuri. Lakini pia anajitahidi kutafuta soko la
muziki nje na kukuza muziki wetu kwa kuutangaza katika soko la
kimataifa.
Nilipoishia mimi kwa wakati ule, yeye amekwenda
mbele zaidi. Najivunia hilo, lakini ajue kwamba, nami ninarudi kwa kasi
ya ajabu.