Dar es Salaam. Tanzania imegoma kuridhia pendekezo linalotaka haki kwa watu wenye uhusiano ya jinsia moja kuingizwa katika sheria z...
Dar es Salaam. Tanzania imegoma kuridhia
pendekezo linalotaka haki kwa watu wenye uhusiano ya jinsia moja
kuingizwa katika sheria za ndani lililotolewa na Baraza la Haki za
Binadamu la Umoja wa Mataifa chini ya mapendekezo ya pamoja ya dunia.
Pendekezo hilo ni kati ya mapendekezo 153
yaliyotolewa kwa Tanzania na baraza hilo Oktoba 2011. Kati ya hayo
Serikali ilikubali mapendekezo 107 na kukubali sehemu fulani tu ya
mapendekezo 13.
Kutokana na hilo jumla ya mapendekezo 33 yalikataliwa na Serikali likiwamo la hilo.
Akizungumza kwenye hafla ya maadhimisho ya Siku ya
Haki za Binadamu Duniani iliyohudhuriwa na mabalozi mbalimbali nchini
pamoja na wadau, Mkurugenzi Msaidizi, Masuala ya Haki za Binadamu katika
ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Nkasori Sarakikya alisema,
baadhi ya mapendekezo yaliyokataliwa ni yale yanayokinzana na utamaduni
wa nchi.
Sarakikya aliongeza kuwa yale 107 yaliyoungwa mkono kwani ni muhimu katika uboreshaji wa haki za binadamu nchini.
Sarakikya alieleza kuwa mapendekezo kama ya kutaka
kutoa haki kwa watu wenye uhusiano wa jinsia moja, kuondoa utaratibu wa
kulipa mahari na ndoa ya mke zaidi ya mmoja, wasichana kuolewa wakiwa
na umri wa miaka 14 pamoja ya kutaka hukumu ya kunyongwa ifutwe hayawezi
kuingizwa katika sheria za ndani.
Lakini alibainisha kuwa, pendekezo la kufuta umri
wa kuolewa na kuufanya ufikie miaka 18 linafanyiwa kazi kwani kwa namna
moja au nyingine linakiuka haki za binadamu.
“Hapo awali tulikataa kwa sababu tusingeweza
kufanya uamuzi sisi wenyewe bila kushirikisha viongozi mbalimbali hasa
wa dini kwani kuna baadhi ya dini zinaruhusu hilo,” alifafanua.
Hata hivyo, alisema kwenye Katiba Inayopendekezwa
suala la umri wa kuolewa limezungumziwa na kwamba mapendekezo
yamepitishwa kuwa umri wa kuolewa uongezwe hadi kufikia miaka 18.
Akisoma hotuba yake, Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU)
nchini, Filiberto Sebregondi alitoa rai kwa Serikali kukubaliana na
baadhi ya mapendekezo likiwamo lile linalopinga wasichana kuolewa wakiwa
na umri mdogo.
“Natumaini kuwa Serikali hii itafikiria na baadaye
kuyapitisha mapendekeo hayo. Mfano suala ya wasichana kuolewa wakiwa na
umri wa chini ya 14. Hilo ni jambo la msingi ambalo linatakiwa
kuzingatiwa kwani linaenda kinyume na haki za binadamu,” alisema
Sebregondi.
Mbali na ombi hilo balozi huyo aliipongeza
Serikali ya Tanzania kwa juhudi ambazo imekuwa ikifanya za kupambana na
mambo mbalimbali yanayohusiana na uvunjivu wa haki za binadamu.
- Mwananchi
- Mwananchi