Makongoro Oging’ na Shani Ramadhan Msaidizi wa kazi za ndani (hausigeli), Rehema A...
Makongoro Oging’ na Shani Ramadhan
Msaidizi wa kazi za ndani (hausigeli), Rehema Ally (17), mkazi wa Yombo, Machimbo Mwisho, Ilala jijini Dar, amechanwachanwa kwa wembe na kisu sehemu mbalimbali za mwili wake, hali iliyosababisha alazwe katika Hospitali ya Amana kwa matibabu.
“Nakumbuka siku hiyo ilikuwa ni Jumapili ya Novemba 30, saa moja usiku nikiwa nje ya nyumba ya bosi wangu. Akatokea msichana mmoja aitwaye Fatuma na mwenzake aitwaye Ashura huku wakiwa wamebeba kisu na wembe. Wakanikamata kwa nguvu na kunikaba, wakaniangusha chini na kuanza kunichanachana mwili mzima.
“Wakati huo nilikuwa naelekea nyumbani kwa akina Fatuma kuchukua sanduku langu ambalo alilichukua kwa bosi wangu akidai kwamba nimempotezea ‘memori kadi’ ya simu yake hivyo alisema kwamba mpaka nitakapomrudishia ndipo nitakapochukua sanduku langu.
“Tulienda kwa mjumbe pamoja na Fatuma na wazazi wake na mimi nilikuwa na bosi wangu, wakataka kesi imalizike yaani tusameheane lakini kwa upande wa wazazi wangu waliopo Masasi, nilipowapa taarifa walikataa kumaliza kesi kienyeji na kutaka ifike mahakamani kwa vile watuhumiwa walikuja na silaha na walidhamiria kuniua,” alisema Rehema.
Kwa upande wa mtuhumiwa, Fatuma Zuberi (17), alipoulizwa na waandishi wetu, alidai kwamba wakiwa njiani na mdogo wake wakienda dukani kununua vocha, walivamiwa na Rehema na kushambuliwa akitaka wamrudishie sanduku lake.