MKE wa aliyekuwa memba wa Kundi la TMK Family, Yessaya Ambikile ‘YP’ aliyefariki katika Hospitali ya Temeke, jijini Dar, Sakina Robert...
MKE
wa aliyekuwa memba wa Kundi la TMK Family, Yessaya Ambikile ‘YP’
aliyefariki katika Hospitali ya Temeke, jijini Dar, Sakina Robert
amefungukia mateso aliyopitia mumewe hadi umauti ulipomkuta usiku wa
Oktoba 20, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wetu nyumbani alipokuwa akiishi na marehemu,
Keko jijini Dar, Sakina alisema mumewe ameteseka kwa muda mrefu
akisumbuliwa na ugonjwa wa kifua kikuu ambapo alitibiwa na kumaliza dozi
kabla ya kuugua ugonjwa wa Pneumonia ambao ndiyo uliomsababishia kifo
chake.
Sakina alisema, awali YP alikuwa akilalamika kubanwa na kifua kiasi
cha kupumua kwa tabu hivyo akashirikiana na familia ya mumewe kumkimbiza
hospitali kwa ajili ya matibabu.
“Mwezi wa tatu mwaka huu, YP aligundulika na ugonjwa wa kifua kikuu
na tayari alianza matibabu, alimaliza dozi mwezi wa tisa na hali yake
ghafla ikabadilika na kuanza kubanwa na kifua. Tulimpeleka Hospitali ya
Temeke, Oktoba 19 mwaka huu na akaonekana ana Pneumonia, Oktoba 20 usiku
ndipo akafariki,” alisema mke wa marehemu kwa uchungu.
Meneja wa Kruu ya TMK Family, Said Fella aliyeambatana na rafiki wa
karibu wa marehemu Said Chigunda ‘Chegge’ alimuelezea YP kama shujaa,
aliyekuwa tayari kupambana muda wote na kuongeza kuwa YP alifariki
wakati akiwa bado hajamaliza kurekodi ngoma yao iliyopewa jina la Wazee
wa Jiji waliyofanya na Kundi la Tip Top Connection.
Enzi za uhai wake, marehemu YP amesikika katika ngoma kali ikiwemo,
Dar Mpaka Moro, Umewaona, Twenzetu Kichwa Kinauma, Umri, Pumzika na
Tunafurahi.
YP alizikwa juzi katika Makaburi ya Chang’ombe jijini Dar, Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Amina.
YP alizikwa juzi katika Makaburi ya Chang’ombe jijini Dar, Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Amina.