Je, upo kwenye uhusiano wa kimapenzi, unampenda sana mume, mke, mchumb...
Je, upo kwenye uhusiano wa
kimapenzi, unampenda sana mume, mke, mchumba au mpenzi
uliyenaye lakini wazazi au ndugu zako wanamchukia na kila
siku wanampiga vita?
Mada
ya leo ni kwa ajili ya wewe msomaji wangu ambaye upo kwenye
mazingira kama haya ya wazazi au ndugu kumkataa umpendaye
kwa sababu ambazo wanazijua leo. Kwa ambao wamewahi kupitia
changamoto hii au bado wapo ndani yake, watakuwa wanaelewa
vizuri ugumu uliopo linapokuja suala kama hili.
Wazazi wako wamekuzaa na kukulea tangu
ukiwa mdogo mpaka umekuwa mkubwa, umempata umpendaye lakini
wao wanamkataa na kukwambia unatakiwa kuchagua moja, wao
(wazazi) au huyo unayempenda. Utachukua uamuzi gani?
Utamuacha kwa sababu wazazi hawampendi? Utakubali kuwadharau
wazazi wako na kuendelea naye?
Bila shaka kila mmoja atakuwa na
jibu lake tofauti, hata mimi ukiniuliza nitakuwa na jibu
langu lakini tunachokihitaji hapa, ni kujadiliana,
kupanuana mawazo, kupeana uzoefu ili mwisho kila mmoja awe
na uwezo wa kuivuka changamoto hii kwa sababu hata kama
bado haijakukuta, huenda ipo siku na wewe yatakutokea.
MFANO HAI
Hebu soma ushuhuda wa msomaji wangu
mmoja ambaye yupo kwenye hali mbaya na anahitaji ushauri:
“Mimi ni mwanaume mwenye umri wa
miaka 42, nilioa miaka kumi iliyopita na tumejaliwa kupata
watoto wawili. Tatizo linalonisumbua na kuniweka njia
panda, mke wangu anawachukia sana wazazi wangu na ndugu
wote kutoka upande wangu.
“Wazazi wangu wamekuja mjini kwa
zaidi ya miezi miwili sasa kwa ajili ya matibabu lakini
huwezi kuamini, mke wangu anawachukia kiasi kwamba hata
salamu kwake ni mtihani.
Anawadharau, wanapishana ndani kama
wake wenza, anazungumza maneno machafu dhidi yao ambayo
mengine nayasikia, hawapi matunzo mazuri, anawanyanyasa na
kibaya anawafundisha mpaka wanangu kuwadharau babu na
bibi.
“Hali hiyo imesababisha wazazi nao
waanze kumchukia sana, wananiambia nimekosea kuchagua mke
na wananitolea maneno makali ambayo mengine hayaandikiki.
Nipo njia panda, sijui niamue nini, bado nampenda mke
wangu lakini mambo anayoyafanya yamesababisha mapenzi
yangu kwake yapungue mpaka nafikiria kumpa talaka ili
kuwafurahisha wazazi wangu. Naomba ushauri, nifanyeje?”
Amehitimisha msomaji wangu huyu, bila
shaka umemuelewa. Najua huyu ni mmoja tu lakini wapo wengi
ambao wanatokewa na visa kama hivi. Naomba tujadiliane
pamoja, ungekuwa ni wewe kwenye nafasi ya msomaji huyu,
ungefanya nini? Kama ungepewa kazi ya kumshauri,
ungemwambia nini?
TAFUTA CHANZO CHA TATIZO
Hakuna chuki ambayo huwa haina
chanzo. Kama mumeo, mkeo anawachukia ndugu zako, jambo la
kwanza ambalo unatakiwa kulijua, ni kwamba lazima kuna
chanzo kilichosababisha hali hiyo. Na kama yalivyo
matatizo mengine yote, huwezi kupata muafaka kama
hujakijua chanzo.
Wengi hushindwa kutumia busara katika
kutafuta chanzo. Yawezekana umpendaye ndiyo chanzo ila kwa
sababu ya mapenzi yako kwake, unaukataa ukweli na
kumtetea.
Itaendelea wiki ijayo.