Mwasiti na Banana Zorro wametangazwa kama mabalozi wa kampeni ya ‘Stand Up For African Mothers’ Mwasiti akiongea na waandishi wa habar...
Mwasiti na Banana Zorro wametangazwa kama mabalozi wa kampeni ya ‘Stand Up For African Mothers’
Mwasiti ameiambia Bongo5 kuwa amesema amefurahi kuchaguliwa kuwa
balozi. “Unajua hii inaonyesha jinsi gani sasa hivi wasanii
tunathaminiwa. Tutakuwa mabalozi wa hii kampeni kwa muda wa mwaka mmoja
na pia tutazunguka Tanzania nzima kutoa elimu,” amesema.
Wanawake 7,900 wa Tanzania hupoteza maisha kila mwaka wakati wa
kujifungua. Zaidi ya asilimia 80 ya vifo hivi vingeweza kuepukika endapo
wahudumu wa afya wenye utaalamu wangetoa huduma kwa wakina mama
wajawazito wakati wa kujifungua. Kwa kuamini kuwa hakuna mwanamke
anayepaswa kufa wakati wa kujifungua, Shirika la Amref Health Africa
Tanzania kwa kushirikiana na Bank za Barclays na Bank M wameonesha nia
ya kuongeza nguvu na juhudi za kutunisha mfuko wa kusaidia mafunzo ya
wakunga kupitia kampeni yake ya Stand up for African Mothers.
Kampeni hiyo ya kimataifa inalenga katika kuongeza uelewa juu ya
mchango unaotolewa na wakunga wenye ujuzi katika kupunguza vifo vya
wajawazito wakati wa kujifungua na watoto wachanga. Kampeni hii pia
inalenga kukusanya fedha kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa wakunga 15,000
katika nchi 13 za Afrika, kati yao wakunga 3800 wanatarajiwa kupata
mafunzo nchini Tanzania ifikapo mwaka 2015/2016. Kauli mbiu ya mwaka huu
ni “Changia mafunzo ya wakunga , okoa maisha ya mama na mtoto” kwa
kuunga mkono nia hii njema unasaidia kuwapatia mafunzo wahudumu wa afya
walio mstari wa mbele kuokoa maisha ya mama na mtoto nchini Tanzania.
Nchini Tanzania kampeni hii ilizinduliwa na Mke wa Rais Mama Salma
Kikwete tarehe 15 Mei mwaka 2012. Mke wa Raisi amekuwa balozi wa kampeni
hii akiongoza juhudi za kuwaokoa kina mama wa kiafrika.