MSHINDI wa shindano la Miss East Africa kwa mwaka 2012, Joselyn Maro amepeleka malalamiko yake kwenye Baraza la...
MSHINDI wa shindano la Miss East Africa kwa mwaka 2012, Joselyn
Maro amepeleka malalamiko yake kwenye Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA)
akilalamikia kutokabidhiwa nakala muhimu za zawadi yake ya gari
alilopewa kama mshindi.
Mrembo huyo alisema jana kuwa tangia apate ushindi wake huo alipewa
gari aina ya Mazda ambalo hadi sasa hawezi kuliendesha kutokana na
kutopewa kadi ya gari hilo. Alisema kuwa hali hiyo kwake imekuwa ni ya
wasiwasi kwa kuwa amelazimika kuliegesha gari hilo nyumbani akisubilia
kukamilika kwa nakala hizo.
Alisema kuwa amekuwa akilazimika kuwasiliana na mratibu wa shindano
hilo kampuni ya Lena Events bila ya mafanikio yoyote. “Mimi nimekuwa
nikimwomba kunisaidia suala hili la gari lakini ushirikiano umekuwa
hakuna kabisa na niliamua kwenda Basata kuanzia mwezi Februari kuomba
kusaidiwa na ndio ninasubiria majibu”alisema mrembo huyo.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Ukuzaji wa Sanaa wa Basata, Vivia Sharua
alikiri kupokea malalamiko ya Miss huyo na kusisitiza kuwa ofisi yake
imekuwa ikifanya jitihada za kumpata mwandaaji huyo bila ya mafanikio.
“Sisi tumekuwa mara kwa mara tukimwandikia barua ya kumuita kwenye kikao
lakini inaonekana kuwa amekuwa akituchenga”alisema Shalua.
“Hilo gari linathamani ya Dola za Kimarekani 18,000 ambazo mmiliki wa
gari hilo naYe alikuja hapa Basata akilalamika kuwa hakupewa sehemu ya
fedha za gari hilo kutoka kwa mwandaaji huyo na yeye anamdai huyo
mwandaaji”.
Aliendelea kufafanua kuwa kutokana na kutolipwa kwa fedha zake
mmiliki aliyetoa gari hili alilazimika kuzuia kadi ya gari ili lisiweze
kuruhusiwa kutumika. Aliongeza kuwa baraza limeamua kumwandikia barua
tena kwa mara ya mwisho mwandaaji huyo wa shindano hilo ikimwita katika
kikao cha tathmini kitakachofanyika Septemba 24 mwaka huu katika ofisi
za basata zilizopo Ilala.
Aliongeza kuwa kwa utaratibu mwandaaji wa shindano anatakiwa
kukamilisha ripoti ndani ya mwezi mmoja tangia kumalizika kwa shindano
lakini imekuwa tofauti kwa mwandaaji huyo ambapo kwa sasa ni takribani
miaka miwili hajafika kwenye tathmini ya shindano lake.
“Kila akiitwa anakuwa na mambo yake mengine na hiyo imekuwa hivyo
kuanzia mwaka 2012 sasa kwa sasa hivi Basata inae mwanasheria wake hivyo
basi huo ndio mwisho wa huu ubabaishaji sisi tutalisimamia hadi huyo
Miss apate haki yake,”alisema Vivia.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni inayoandaa shindano hilo, Lena Events
Lena Calist alisema kuwa ofisi yake inaendelea kulishughulikia suala
hilo. “Kamati yangu ya ufundi kwa sasa inaendelea na kulishughulikia
suala hilo kwa na kila kitu kitakuwa sawa,”alisema Calist. Alisema kuwa
aliwahi kuitwa Basata kipindi kilichopita na lakini hata hivyo alikuwa
tayari kwenda kwenye kikao hicho kikaahirishwa.