Nyuma ya tukio la denti wa darasa la tano kwenye shule moja ya msingi iliyopo Mbezi-Shamba, Dar, aliyejitambulisha kwa jina moja la Ire...
Nyuma ya tukio la denti wa darasa la tano kwenye shule moja ya msingi
iliyopo Mbezi-Shamba, Dar, aliyejitambulisha kwa jina moja la Irene (11)
la kunaswa akifanya utapeli kwa kuwaibia raia, mazito yameibuka.
Katika tukio hilo lililojiri hivi karibuni maeneo ya Posta Mpya, Dar,
denti huyo alikuwa akisimama nyakati za asubuhi akivalia sare za shule
huku akiombaomba kwa madai kuwa hana nauli ya kuvukia katika kivuko cha
Kigamboni kwenda shule anayosoma.
Kwa mujibu wa mmoja wa mashuhuda, mtoto huyo alikuwa akisimama mbele
ya Kituo cha Daladala cha Posta mpya akijifanya ombaomba kwa madai
kwamba hana nauli.Ilisemekana kwamba siku nyingine mtoto huyo alikuwa
akionekana akiuza simu kwa bei chee na alipohojiwa alikokuwa akizitoa
alidai ameziokota.
Dereva mmoja, Juma Hamis anayeegesha gari lake eneo hilo (Posta Mpya)
alisema kuwa tabia ya mtoto huyo ilikuwa ni ya muda mrefu kwani
alianzia Kariakoo, Dar akitapeli na kuiba madukani ambapo watu
walimstukia hivyo akaamua kuhamia Posta.
“Mara kadhaa amenusurika kupigwa akidaiwa kuchomoa simu za watu
kwenye mikoba ndani ya daladala.“Kukamatwa kwa Irene, watu wa maofisini
na kwenye daladala wameshukuru kwani anafahamika na ni tishio kwa
utapeli na ndiyo waliomchoma kwa polisi akadakwa baada ya kukutwa
akijidai ni ombaomba,” alisema dereva huyo.
Jader Sapi, anayefanya kazi katika ofisi moja zilizo ndani ya jengo
la IPS, alisema mtoto huyo aliwahi kuingia ofisini kwao na alipotoka,
wafanyakazi wawili walilalamika kupotea kwa simu zao, kitu
kilichowafanya wajue ni yeye.
Mama mmoja aliyeshuhudia Irene akichukuliwa na askari, alisema
ameshawahi kumpa fedha mara kadhaa denti huyo, akiamini alivyomweleza
kuwa hakuna na wazazi na hivyo hana nauli ya kumpeleka shuleni.
Akizungumza na gazeti hili akiwa mikononi mwa polisi kwenye Kituo
Kikuu, Irene alisema ni mwanafunzi wa shule moja ya msingi (jina kapuni)
iliyopo Mbezi-Shamba na siyo kama alivyokuwa akidanganya kuwa anasoma
Kigamboni, Dar.
Pia alikiri kwamba amekuwa akidanganya kuwa hana wazazi wakati ukweli
ni kwamba wazazi wake wapo.“Ni shetani tu aliniingia nikawadanganya
raia,’’ alisema Irene.
Baada ya kushuhudia tukio hilo, wanahabari wetu walimsaka mkuu wa
shule anayosoma mtoto huyo, Yusuph Zenny ambaye alikiri kumfahamu Irene
na kudai kuwa tayari taarifa kutoka Kituo Kikuu cha Polisi, Dar
zilimfikia.
Alitobosa siri kuwa ameshapata malalamiko mara kadhaa kuhusiana na
binti huyo na kwamba amekuwa akifanya uchunguzi ili kupata ukweli.
Hata hivyo, alisema anawasiliana na wazazi ili kulifuatilia sakata
hilo hivyo kuwaomba wanahabari wetu wampe muda atatoa majibu au hatua
itakayochukuliwa huku Irene akiwa bado mikononi mwa polisi kwenye dawati
la jinsia.