Add caption TUNAKUTANA tena leo katika safu yetu hii maridhawa, wakati huu ambao...
Add caption |
TUNAKUTANA tena leo katika safu yetu hii maridhawa, wakati huu ambao vijana wetu wa darasa la saba tayari wameshafanya mitihani.
Kwanza niwapongeze wanangu wa darasa la saba kwa kazi kubwa na nzuri
waliyofanya kwa kipindi chote wakiwa shuleni hadi juzi walipohitimisha
kwa mtihani wao wa mwisho. Niwape pia moyo wa matumaini vijana wetu wa
kidato cha nne kuelekea katika mitihani yenu ya kumaliza ngazi hiyo
muhimu kabisa katika maisha.
Baada ya kusema hivyo, sasa tuje katika mada yetu ambayo kwa kiasi
chake ni muhimu sana kwa wanafunzi wetu wa kizazi cha sasa ambao usafiri
wa daladala kwao haukwepeki, hasa kutokana na shule nyingi kuwa mbali
na maeneo ya makazi yao.
Wote tunajua kuwa lipo tatizo kubwa sana la usafiri kwa wanafunzi,
hasa jijini Dar es Salaam kwani wafanyakazi wa kwenye mabasi, ambao sisi
tunawaita makonda, wengi wao ni wasumbufu. Binafsi kuna wakati huwa
nakereka sana ukiwa kwenye daladala halafu ukaona jinsi wanafunzi
wanavyozuiwa kuingia katika daladala.
Kama kwa mfano kituo kina wanafunzi wengi, magari huwa hayasimami na
hata pale wanapolazimika kusimama kwa sababu ya abiria anashuka, bado
makonda utawakuta wanawazuia kwa nguvu sana wanafunzi. Huwa najiuliza,
hivi hawa hawana watoto wanaosoma?
Lakini hata hivyo, kuna kipindi huwa nalazimika kuwachukulia poa tu
makonda wanavyofanya, kutokana na baadhi ya vitendo visivyoridhisha vya
baadhi ya wanafunzi wakiwa ndani ya haya magari ya daladala.
Utakuta wanafunzi wamepanda kituo kimoja labda watano, kitu ambacho
pia huwa kinawakera sana makonda, wakiwa ndani sasa, wanaongea kwa sauti
ya juu kana kwamba wako peke yao. Halafu mbaya zaidi, wakati mwingine
wanazungumza maneno ambayo hayastahili, hasa kwa kuzingatia kuwa ndani
ya magari hayo, wapo baba na mama zao, kaka na dada zao na hata wajomba
na shangazi zao, ambao ni wakubwa kiumri na hivyo walipaswa kuheshimiwa!
Lakini zaidi ya yote, kuna hili la wanafunzi kuanzisha bifu la
makusudi na makonda, ili mradi tu kuwaonyesha kwamba wao ni nani.
Juzikati nilikutana na hiki kitu ndani ya gari, nikaumia sana, kwa
sababu ninajua wazazi wanatokwa na jasho jingi sana kwa ajili ya
kuhakikisha watoto wao wanapata elimu bora, lakini kinachofanywa na
watoto hawa wakati mwingine hakipendezi kabisa.
Konda wa gari tulilopanda alikuwa mstaarabu kiasi cha kutosha, kila
kituo alisimama na alipakia wanafunzi wengi kuliko kawaida. Tatizo
likaja wakati akianza kutoza nauli. Huwezi kuamini, wanafunzi kama
watano hivi wa kiume, wakamwambia hawana hela!
Kukosa hela ya nauli kwa mwanafunzi ni jambo la kawaida kwa sababu
hata sisi wafanyakazi wenyewe wakati mwingine huwa tunabanwa, lakini
unapokuwa katika hali hiyo, ni lazima uonyeshe hivyo kwa konda kwa
sababu yeye yupo kazini!
Kwa hiyo wakampa kwa sauti ya juu kabisa na kujiamini; “Wewe si
unatuona sisi wanafunzi, hatuna kazi halafu unatudai nauli, wee boya
nini?”
Dah, aisee nilitamani kununua kesi, yaani huna nauli halafu unaleta
maneno ya nyodo. Baada ya majibishano kati ya konda na wale madenti kama
dakika moja hivi, ghafla basi zima wakawa upande wa konda, wakaanza
kuwananga wale wanafunzi na wakaamuru gari lisimamishwe washushwe, mbona
walilipa nauli!