Wiki iliyopita Nature alielezea ujio wa kundi jipya la Wanaume Halisi baada ya kuvunjika kwa Kundi la Wanaume Family. ...
Wiki iliyopita Nature alielezea ujio wa kundi jipya la Wanaume Halisi baada ya kuvunjika kwa Kundi la Wanaume Family.
Wiki hii pamoja na mambo mengine, nguli huyo wa
muziki wa kizazi kipya anaeleza jinsi alivyopata wakati mgumu kutunga
mashairi na hali ya muziki ilivyo.
Anaeleza kuwa iliwachukua siku nyingi kutunga
mashairi la wimbo mmoja na kwamba walifanya hivyo ili zidumu, hivyo
shairi moja lilikuwa likimchukua hadi mwezi mzima kukamilisha kulitunga.
“Labda uwezo wetu ulikuwa mdogo, naona siku hizi
mtu anatunga nyimbo 12 kwa siku. Mimi huwa nashangaa sana, au msanii
mchanga anakwambia ana albamu nne ingawa inasikika kwa singo
moja,”anasema Nature.
Anasema kuwa ugumu wa kazi hiyo ulimfanya hata
augue homa kila alipomaliza kutunga nyimbo za albamu, kutokana na uchovu
uliotokana na kuishughulisha akili bila kutaka kubugudhiwa. Nature
anaeleza kuwa ilifikia wakati alikwenda kushinda ufukweni mwa bahari ili
kukimbia marafiki ambao wangemsumbua wakati anatunga mashairi.
“Hakuna albamu niliyotunga bila kupata homa, hasa
ya ‘Ugali’ ndiyo niliumwa sana, ndiyo sababu nikiona mtu ametunga nyimbo
zaidi ya 10 kwa siku, namshangaa na kuona ana uwezo sana, “anasema
Nature.
Nature anazungumzia utunzi wa sasa na mapokeo ya
mashabiki akisema kuwa watunzi wengi hurudia ujumbe kutokana na kukosa
umakini na kuiga, hivyo kutodumu na kuyeyuka mapema mioyoni mwa
mashabiki.
Anafafanua kuwa wasanii wengi wa muziki kwa sasa
wanaamini wakiimba singo moja watakuwa matajiri kutokana na kuwaona
baadhi ya wanamuziki wamefanikiwa na wao kutamani hali hiyo, lakini
matokeo yake wanaboronga.
Anaitaja changamoto wanakumbana nayo wasanii kwa
sasa kuwa ni wanaojiita wadau wa muziki wa kizazi kipya kuwatumia vibaya
wasanii na wanang’amua wanatumiwa, hupotezwa katika sanaa.
Anasema hali hiyo imekuwa inawaondoa kwenye soko wasanii mahiri kwa sababu watu wanaowaamini huwanyonya na kuwaacha hoi.
“Hapa nawataka wasanii wenzangu kuwa makini na
watu hawa wanaojifanya wanapenda kuendeleza muziki na wasanii kwani
mwishowe huwapoteza makusudi katika sanaa ili kujilinda wasionekane
wabaya, “anasema.
Kuhusu kuwapo kwa studio nyingi za muziki ikiwamo
ya kwake ( Halisi Recods), Nature alisema kuwa zinaleta ushindani
unaozaa kazi bora
- Mwananchi