WAKATI matukio mengi ya kushangaza na kushtukiza yakiendelea kutokea kila siku du...
WAKATI matukio mengi ya kushangaza na kushtukiza yakiendelea kutokea kila siku duniani, neno la Mungu nalo linazidi kushika kasi kufuatia baa moja iliyopo Sinza-Lion jijini Dar kugeuzwa kuwa kanisa.
Baa iliyopo Sinza-Lion jijini Dar ambayo imegeuzwa kuwa kanisa.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili
umebaini kuwa baa hiyo maarufu iitwayo The Don, ukumbi wake ambao
ulikuwa ukitumika kwa watu kupiga ulabu, hivi sasa unatumiwa na waumini
wa kanisa linalojukana kama Impact International Christian Centre kupata
mahubiri.
Lakini cha kushangaza ilibainika kwamba
katika maandishi makubwa yanayolinadi jina la baa hiyo, chini yake ndipo
limewekwa bango linaloonyesha kanisa hilo, kitu ambacho kwa mtu mgeni,
ni vigumu kuelewa mara moja.
“Siyo baa hiyo kaka, hilo ni kanisa siku hizi, tumeshangaa ghafla tu
waumini wanakuja na mhubiri wao na wanaendelea na sala kama kawaida.
Hatujui kama huyu mhubiri ndiye alikuwa mmiliki wa hii baa au
imekuwaje,” alisema jirani mmoja wa eneo hilo, aliyekataa kutaja jina.
Hata
hivyo, juhudi za gazeti hili kuzungumza na uongozi wa baa au kanisa
hilo ziligonga mwamba baada ya kuambiwa na majirani kuwa ni nadra
kuwakuta mahali hapo hivyo jitihada zinaendelea.
Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na wimbi kubwa la kuibuka kwa
makanisa ya madhehebu mbalimbali, ambayo kila moja huwa na watumishi wao
wanaopewa majina kama Mchungaji, Nabii, Askofu na kadhalika.