Clouds media International yenye makao yake makuu Abu Dhabi, imefungua ofisi mpya huko Kingston Jamaica zitakazohudumia ukanda wa Caribb...
Clouds media International yenye makao yake makuu Abu Dhabi,
imefungua ofisi mpya huko Kingston Jamaica zitakazohudumia ukanda wa
Caribbean na kufungua fursa za kibiashara kwa kampuni tanzu za Clouds
Media.
Ufunguzi wa ofisi mpya nchini Jamaica unakuja ikiwa hata mwaka mmoja
haujapita toka Clouds Media International ilipofungua ofisi zake Abu
Dhabi.
Mkurugenzi mtendajib wa Clouds Media, Joseph Kusaga amesema ufunguzi
huu ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu kuiwezesha kampuni yake kujitanua
kimataifa ikiwa ni pamoja na uzalishaji na usambazaji vipindi, utoaji
wa huduma za ziada kupitia simu za mkononi, masoko na usimamizi wa
matamasha bila kusahau matumizi ya solar na vyombo vya habari.
“Jamaica na Caribia kwa ujumla ni soko jipya kwetu na kama Clouds
mara zote huwa tunafikiria ni kwa namna gani tunaweza kujipenyeza
katika masoko mapya ili kujitanua na kufanya biashara endelevu hivyo
tunaona hii ni sehemu ya muafaka wa bidhaa na huduma tunazotoa” – Joseph Kusaga.
Shughuli zote za Clouds International zitasimamiwa na Dean Mundy,
mtayarishaji wa muziki wa reggae na mfanyabiashara mzawa wa Jamaica
mwenye uzoefu katika ukanda huo ambapo kukamilika kwa uzinduzi wa ofisi
hizi kunadhihirisha umakini wa Clouds kujitanua kimataifa.
“Ni zaidi ya muongo mmoja sasa toka nilipokutana na Joe na
wenzake nilipokuja Dar es salaam kwenye tamasha la Fiesta na
haikunichukua muda kutambua kuwa hii ni kampuni ambayo tunaweza kufanya
nayo kitu, japo kwa hakika sikujua ni kivipi ila kwa sasa uhakika ninao
na pia fursa zipo, tuko tayari kufanya vitu vikubwa hapa Jamaica” – Mundy
Pamoja na Clouds Media International, makampuni tanzu kama status
communications, Primetime International na Ray’s Solar yatakua na makao
yake Kingston, ambapo status communications itajihusisha na utoaji
huduma za ziada kupitia simu za mkononi, Primetime International
itasimamia uandaaji wa matamasha na usimamizi wa Wasanii huku Ray’s
Solar ikitoa huduma za umeme wa mionzi ya jua.
Source: CloudsFm