Huduma ya usafiri wa treni ya abiria kuelekea bara zinaanza rasmi leo, huku, Kampuni ya Reli ya Tanzania (TRL) ikiwahakikishia...

Usafiri huo ulisitishwa Januari 10, mwaka huu baada ya kuharibika kwa miundombinu ya reli
kutokana na mvua kubwa zilizokuwa zikinyesha.
Meneja Mkuu wa Masoko wa TRL, Charles Ndenge alisema hayo Dar es
Salaam jana.
“Takribani miezi mitano imepita tangu kusitishwa kwa huduma hiyo, uamuzi
wa kuanza kutoa tena huduma leo unatokana na kukamilika kwa kazi ya ukarabati
wa reli eneo la kati ya stesheni za
Kilosa mkoani Morogoro na Gulwe mkoani Dodoma,” alisema .
Aidha alisema licha ya TRL
kutangaza kuanza upya kwa huduma hiyo na kuwataka wasafiri kukata tiketi
kuanzia Mei 22, mwitikio umekuwa wa
wastani katika baadhi ya vituo.
Alifafanua zaidi kuwa katika
safari zitakazoanza leo, mizigo inayozidi uzito wa kawaida itafanyiwa utaratibu
wa kusajiliwa mapema ili kuweza kusafirishwa katika behewa la breki siku moja
kabla ya safari husika.
Meneja Mkuu wa Usafirishaji, Rowland Simtengu alisema kampuni hiyo
imejiandaa vya kutosha kukidhi matakwa ya huduma na haitarajiwi kuwepo kwa
usumbufu wa aina yoyote wala vitendea kazi.
Kuhusu siku za safari alisema zimebakia kama zilivyo; Mara mbili ambapo
kwa treni ya kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma na Mwanza ni Jumanne na Ijumaa
wakati zinazotoka Kigoma na Mwanza kwenda
Dar es Salaam ni Alhamisi na Jumapili.