Arusha. Katika jamii nyingi, hasa za mijini, ni kawaida wanawake na wanaume kushirikiana katika shughuli mbalimbali za kiuch...
Arusha. Katika jamii nyingi, hasa za mijini, ni kawaida wanawake na wanaume kushirikiana katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Lakini hali hii ni tofauti kwa Wanawake wa jamii za pembezoni za wafugaji; Wamasai, Wabaebeig na Wahadzabe ambao wanaume wao badala ya kuwaunga mkono katika miradi yao, wamekuwa wakiwahujumu.
Baadhi ya wanaume hawa wamefikia hatua ya kupora mifugo, ya vikundi vya akina mama hawa, ili wasiendelee kiuchumi.
Wanawake wa jamii hizo, wakizungumza
na Mwananchi katika mkutano uliokuwa umeandaliwa na mtandao wa mashirika
ya wafugaji na waokota matunda (PINGOS Forums), wanasema miradi yao
imekufa baada ya kuhujumiwa na waume zao.
Amina Msendekwa, mfugaji kutoka jamii
ya Wamasai wa Kijiji cha Wami Sokoine wilayani Mvomelo, anasema mradi
wao wa kunenepesha mifugo katika kijiji chao umekwama baada ya wanaume
wao kuiba mifugo kabla ya mauzo ili wasiendelee na biashara hiyo.
Anasema walianzisha mradi huo baada ya
kupata hamasa na elimu ya kutosha, hivyo wakawa wananunua ndama wadogo
na kuwafuga kwa kuwanenepesha na baadaye kujipanga kuuza ng'ombe
wakubwa.
"Mradi wetu ulikuwa mzuri sana.
Tulinenepesha mifugo, lakini tulipopanga kuuza baada ya kukamilika,
tulianza kuibiwa kidogo kidogo," anasema.
Kutokana na majukumu yao kama
wanawake, iliwalazimu kuomba msaada kwa wanaume kuwasaidia kuwasaka
ng'ombe waliokuwa wanaibiwa, lakini cha ajabu walikuwa hawapewi
ushirikiano na baadaye walibaini ni njama za waume zao.
"kila tulipokuwa tukipanga kupeleka
ng'ombe mnadani, waliibiwa na wanaume zetu na jitihada za kurejeshewa
zilikwama hadi sasa mradi umekufa," anasema Msendekwa.
Paulina Tipapu, mkazi wa Loliondo,
anasema licha ya mtandao wa mashirika yasiyo ya kiserikali wilaya ya
Ngorongoro wa Nngonet kuwapa mbuzi watano wa kisasa, mradi huo
umekwamishwa na wanaume.
Tipapu anasema wanaume wamekuwa
wakichukuwa mbuzi bila idhini yao na kwenda kuwauza na hata pale
wanapokwenda wao kuuza wanaume wamekuwa waking'ang'ania fedha.
"Tumeshindwa kuendeleza mradi kama
tulivyotarajia baada ya waume zetu kutuhujumu. Sasa tunakaa kubuni
miradi mingine," anasema Tipapu.
Chanzo Mwananchi